KINACHOWASHANGAZA
ni kipi enyi walimwengu? Natamani nianzishe intelijensia yangu ili haya mambo
yanayowaumiza vichwa yafikie ukomo.
Naapa
ni intelijensia tu ndio inaweza kuwapa ufafanuzi wa haya mambo yanayowakereketa
bila majibu au suluhisho mwafaka.
Nasema
ngoja tu siku Katiba mpya itakaporuhusu watu binafsi kuanzisha intelijensia zao
zifanye kazi sambamba na zile za polisi ndipo mtajua namaanisha nini.
Hizi
intelijensia za polisi kila mara wakitutangazia si zinahusika na haya mambo ya
vyama vya siasa? Zao mara nyingi tumesikia zikibashiri uwepo wa vurugu pindi
maandamano yakifanyika au michakato kama hiyo.
Huko
mimi siko, niko kwenye hii intelijensia ninayoitamani kuanzisha.
Mwanangu
kama ningepewa ruhusa ningeanza kwa kuanzisha intelijensia ya kuchunguza
madhara ya mikataba kabla haijatiwa sahihi.
Mmenisoma
hadi hapo au mnashangaa shangaa tu? Kama ile intelijensia ya polisi inavyoweza
kubashiri kwa hakika kwamba watu wakitembea zaidi ya kilomita mbili pamoja kuna
nafasi kubwa ya vurugu kutokea, hii ya kwangu itabashiri kwamba mikataba
iliyoingiwa kimizengwe ina hatari kubwa ya kuliletea taifa hasara itakayolipwa
hadi na vilembwe wetu. Huko simo mtoto wa mama miye.
Intelijensia
yangu isingehangaika sana na mambo ya kisiasa. Ingeanza kuwamulika hao watu
wanaoitwa wawekezaji na kujua kama huko walikotoka wana walau baisekeli.
Mnabisha
nini? Hamkusikia kuna lijikampuni limevuna kwetu kama vile ni shamba la bibi
wakati huko kwao tunaambiwa haimiliki hata bajaji?
Mtashangaa
sana na mtakasirika zaidi mkijua wajinga ndio waliwao. Intelijensia yangu
nasema isingedili na maandamano wala mikutano.
Waache
waandamane hadi magoti yaume na wapayuke hadi makoo yawakauke. Hayo
yasingenihusu.
Kwangu
mimi ningedili zaidi na kuangalia hao wanaokuja kuwekeza kwetu wana uaminifu
kiasi gani na tunapata maslahi gani kuwekeza kwa watu hao. Hiyo ndio
intelijensia ninayotamani niruhusiwe kuianzisha.
Mimi
kama ningekuwa na uwezo wa kuwa na intelijensia yangu ningejiingiza pia katika
kuchunguza uozo uliofanyika ambao vyombo vingene vimeshindwa kuuweka hadharani.
Mtu
anaweza kuzoa bilioni arobaini kwa makaratasi ya kughushi halafu inteleijensia
zetu bado hazijampata mtu huyo? Ina maana hizo hela zililipwa na nani?
Yawezekana
siku hizi kuna akaunti zisizo na signatoriz? Nauliza mniambie ninyi mlioshindwa
kukamata waliokwapua mabilioni kwa jina la Kagoda, hizo hela zilichukuliwa na
mizimu? Mimi simo tena simo kabisa.
Hayo
ya Musa, shuruti na ya Firauni muyaone. Mimi nikiangalia hili la kuvunja
mkataba halafu unaambiwa ulipe kuliko ambavyo ungelipa kama mkataba
ungemalizika nalo linahitaji intelijensia ya Mzee wa Kujitoa! Kwani si nasikia
kitivo cha kwanza kuanzishwa pale mlimani ni kitivo cha Sheria? Kitivo cha
sheria si kinapaswa kuzalisha wanasheria? Walikuwa wapi wakati wa uvunjaji wa
mkataba na baadae wakati kashirika ketu kameburuzwa mahakamani?
Nasema
mimi Mzee wa Kujitoa ningekuwa Mzee wa Intelijensia ningeweza kuwashauri hawa
jamaa au wasivunje mkataba au wakivunja ningeweza kubashiri matokeo ya kesi
hivyo kuliokolea taifa fedha.
Maadam
hamnipi hiyo nafasi ya kuunda intelijensia kabila hiyo basi walau tunaomba huko
polisi kuwepo pia na intelijensia ya kujua mambo anayotuletea hasara na hasira.
Simo huko tena nasema simo kabisa. Najitoa mbio kwenye haya yote.
Kama
ningepata nafasi ningeanzisha kitengo kidogo cha intelijenisa kwa ajili ya
kukishauri chama nambari wahedi. Hiki kitengo cha intelijensia kingemshauri
mwenyekiti wa chama hicho kusoma alama za nyakati na kumchagua mtendaji
anayeendana na nyakati.
Kwa
wakati huu unadhani chama hicho kilichopo ICU kina mtendaji anayeweza kupambana
na changamoto zinazokikabili chama?
Mie
simo ila badala ya kunukuu vitabu vya dini asivyovifahamu maana yake, ingekuwa
bora zaidi akatumia katiba ya chama chake kutetea hoja.
Simo
ila wanasema uzee ni dawa. Labda naye kapewa wadhifa huo ili awe dawa. Simo
tena nakimbia mbio kwenye hili.
Lakini
nawaapia kuna intelijensia moja muhimu zaidi ambayo Mzee wa Kujitoa angependa
kuianzisha.
Hii
ni intelijensia ya Mzee wa Kujitoa ya kuwaarifu watu kwamba kama tuatendekeza
udini lazima tutakuja kugeuziana kibao hapa.
Mnadhani
ninyi mnapikia Mola chai hadi mcheze na imani za watu kwa maslahi ya kisiasa
bila kupata adhabu? Bisheni lakini nawaambia kwa udini huu unaoletwa mchana
kweupe, tusije tukashangaa mito ya damu ikianza kutiririka.
Huu
ni udini unaotumiwa na wale ambao wakiutumia kwa akili zao wanadhani watapata
faida za kisiasa.
Hapa
ndipo wanapomkufuru Mungu! Wanatumia dini kisiasa? Wallahi nawaambia tumefika
pabaya. Nikimbie kabla huo ubaya haujanikuta.
Haya
mambo tunayachezea kwa vile hatujawahi kuyashudia kwetu sio? Watu wa kawaida
wala hawana shida ya udni, udini uko kwa wakubwa nakuapia.
Kwetu
mbona Ahmedi anamwoa Mariana na hakuna shida? Kwa watu wa kawaida mbona unakuja
Jamal anacheza na kutaniana kamisa na Dominiki?
Nasema
huu udini huu unaletwa na watu walioshindwa kisiasa. Simo ila kwa nguvu ya
pamoja tunaweza kuwazomea wanaoleta udini na kudumisha tunu yetu ya jadi ya
amani na utulivu.
Mimi
simo ila tujifunze kwa waliopitia kwenye shida kama hizo wanatushangaa
tunapochezea amani kwenye tundu la choo. Nasema tena huku lazima nijitoe
mwanawani.
Nasema
kama ningekuwa na nafasi ya kuanzisha intelijensia yangu ningeanzisha pia ya
kuwatangazia watu kwamba ukisajili wanafunzi wengi vyuo vikuu bila mipango
thabiti lazima itatokea migomo.
Aidha
intelijensia yangu ingegundua kwamba usipowalipa wahadhiri na wasomi mishahara
mizuri au watakimbilia nje ya nchi au wataacha taaluma zao na kuingia kufanya
mabo yasiyo hasa yaani “si hasa.”
Simo
ila ndivyo ambavyo intelijensia yangu ingegundua. Isitoshe intelijensia yangu
ingegundua kwamba ucheleweshaji wa mikopo au kushindwa kutoa mikopo kungeleta
adha kubwa kwa wanafunzi na familia zao hivyo kwa taarifa hizo za
kiintelijensia, mimi Mzee wa Kujitoa nisingesita kupiga marufuku ucheleweshaji
wa mikopo au kuwanyima mikopo wanafunzi wenye sifa husika. Naapa tuunde katiba
mpya. |
No comments:
Post a Comment